بسم الله الرحمن الرحيم

MAJINI

 5

Je kulikuwepo na Majini mitume / manabii? Utume wa Mtume Muhammad (SAW) ni kwa Majini na Wanadamu wote, Mila na madhehebu ya Majini, je Majini wanalipwa kutokana na vitendo vyao?

 

Sheikh Mustafa Mohamed Kihago

 

HOME

 

MAJINI 1 MAJINI 2 MAJINI 3 MAJINI 4 MAJINI 5 MAJINI 6 MAJINI 7 MAJINI 8 MAJINI 9

 

 Bonyeza hapa kusoma maudhui ya kila makala

 

Shukrani za dhati zimwendee Allah (SWT). Pia rehema na amani ziwe juu ya kipenzi chake Muhammad (SAW), pamoja na masahaba wake wote.

 

Majini ni viumbe miongoni mwa viumbe wa Allah (SWT) ambao wamepewa majukumu ya kiibada, lakini majukumu yao ya kiibada hayalingani sawa na majukumu ya kiibada waliyopewa wanadamu isipokuwa majukumu yao yanafanana na ile hali yao ya kimaumbile walioumbiwa. Anasema Ibn Taimiyah: "Majini wameamrishwa katika mambo ya kimsingi katika ibada kwa maumbile yao. Kwani wao hawapo sawa sawa na wanadamu katika hukumu za kidini, haiwezekani kuwa waliyoamrishwa na waliyokatazwa yawe sawa sawa na yale waliyoamrishwa na kukatazwa wanadamu. Lakini tu wao wanashirikiana na wanadamu katika ile hali ya kuwa wao pia wamepewa majukumu ya kidini, kama mambo ya halali, haramu n.k. Hili kwa ninavyofahamu halina utata kwa waislam wote." [ Majmuu'atil - Fataawiy 4:233 ]

 

1. Je kulikuwepo na Majini mitume / manabi ?

 

Swali hili aliulizwa Adhwihaak ya kwamba, je kuna waliokua mitume au manabii miongoni mwa majini kabla ya Mtume Muhammed (SAW)? Akajibu kwa kusema, "Hivi hamkusikia tamko la Allah (SWT) lisemalo 'Enyi makundi ya majini na wanadamu, Je hawajakufikieni Mitume miongoni mwenu kukubainisheni aya zangu ..' Al - An'am 130." Aya hii kwa alivyoona Adhwihaak inafahamisha ya kwamba Allah (SWT) alipeleka majini wakiwa ni Mitume. Lakini yeye amepingwa kwamba hii aya haikuweka wazi mitume waliyotajwa walikua ni katika jamii ipi mojawapo, majini au watu, kwa sababu neno lake Allah (SWT) "miongoni mwenu" inawezekana kwamba mitume walitumwa katika jamii zote hizo mbili na inawezekana ikawa mitume walikuwepo katika jamii moja lakini kwa wote hao. Katika jambo hili wanazuoni walitofautiana katika makundi mawili wengi wao walikubaliana ya kwamba mitume hawakuwepo katika jamii ya majini kamwe, mitume walikuwepo tu katika jamii ya wanadamu.Ni wanazuoni wachache tu ndio walioonelea kwamba kulikuwepo na mitume waliyopelekwa katika jamii ya majini, na miongoni mwa walioonelea hivyo ni huyu mwanazuoni aitwaye Adhwihaak.

 

2. Utume Wa Nabii Muhammad (SAW) kwa majini na wanadamu

 

Wanazuoni wote wa kiislam wamekubaliana kwamba Muhammad (SAW) alitumwa na Allah (SWT) kwa majini na watu wote. Na hivi ndivyo ilivyo kama asemavyo Ibn Taymiyah - kwani Qur-an inashindana na jamii ya majini na pia jamii ya wanadamu. Allah (SWT) anasema: "Sema hata wakijikusanya majini yote na watu wote, ili kuleta mfano wa hii Qur-an, basi hawangaliweza kuleta mfano wake, hata kama watasaidiana wao kwa wao." Al - Israa 88. Na kundi mojawapo la majini lilisilimu mara tu baada ya kusikia Qur-an tukufu: "Sema imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikia Qur-an likasema ( kundi hilo ), 'Hakika sisi tumesikia Qur-an ya ajabu inayoongoza kwenye uongofu, tukaiamini, na kamwe hatutamshirikisha Mola wetu na yeyote yule ....'" A1 - Jinn 1 - 2. Aya zote hizi za Qur-an zinafahamisha wazi kwamba Mtume (SAW) alitumwa kwa majini na watu wote. Ama kuhusu upande wa hadithi za Mtume (SAW) kuna uthibitisho wa wazi katika sahihi mbili Bukhari na Muslim kutokana na hadithi ya Jabir bin Abdallah (RA) kwamba Mtume (SAW) amesema: "Nimepewa mambo matano ambayo hajawahi kupewa Mtume yeyote yule kabla yangu - Mpaka alipofikia: Na kila Mtume alikua akipelekwa kwa kabila lake tu lakini mimi nimetumwa kwa watu wote." Na akasema Jauhariy kwamba makusudio ya watu wote hapa ni kwa majini na wanadamu wote pamoja. Hivyo basi Mtume Muhammad (SAW) alitumwa kwa wanadamu wote pamoja na majini akiwa ni Mjumbe Mwonyaji. Na huu ndio ubora wake uliowazidi mitume wote waliotangulia.

 

3. Mila na madhehebu ya majini

 

Allah (SWT) ametufahamisha ndani ya Qur-an aliposema, "Katika sisi wapo ( majini ) wema na kuna miongoni mwetu ( majini ) kinyume na hao tumekua njia mbali mabli." Al - Jinni 11. "Nasi ( majini ) wamo miongoni mwetu waislamu na wamo miongoni mwetu waliokengeuka. Waliosilimu hao ndio waliotafuta uongofu. Na wanaokengeuka hao watakuwa kuni za Jahannam." Al- Jinn 14 - 15 . Hivyo basi Allah (SWT) katufahamisha kwamba majini nao wana mila na itikadi tofauti kama vile wanadamu walivyo, kuna waislam, makafiri na madhehebu mbalimbali.

 

4. Je majini nao wanalipwa kutokana na vitendo vyao?

 

Wanazuoni wanatofautiana katika hili. Kuna pande mbili za maoni:

 

Upande wa kwanza: unaona kuwa majini watalipwa kwa wema watakaoufanya, na wataadhibiwa kwa maasi yao na hayo ni maoni ya Imam Malik, Shafii, Ahmad na Ibn Abbas.

 

Kundi la pili: linaona kwamba majini hawatakuwa na malipo yeyote isipokuwa kukombolewa na moto wa Jahannamu. Kisha wataambiwa wawe mchanga kama vile itakavyokuwa hali ya wanyama. Na hayo ni maoni ya Imam Abu Hanifa, Laith, Abu Salim na wengineo.

 

Lakini usahihi ni kwamba majini watalipwa kwa vitendo vyao vizuri au vibaya kwa ushahidi wa Qur-an, Allah (SWT) anasema: "Na wote wana daraja ( malipo ) sawa kwa yale waliyoyatenda. Na Mola wako si mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda." Al - An'am 132. Na toleo lijalo litahusu majini katika maisha yao ya kijamii.

 

 

WABILLAHI TAWFIQ

 

و بالله التوفيق