بسم الله الرحمن الرحيم

MAJINI

 9

Sababu kuu ya uadui kati ya Iblis na Mwanadamu, maasi yanayompendeza Iblis zaidi

 

Sheikh Mustafa Mohamed Kihago

 

HOME

 

MAJINI 1 MAJINI 2 MAJINI 3 MAJINI 4 MAJINI 5 MAJINI 6 MAJINI 7 MAJINI 8 MAJINI 9

 

 Bonyeza hapa kusoma maudhui ya kila makala

 

Shukrani za dhati zimwendee Allah (SWT). Pia rehema na amani ziwe juu ya kipenzi chake Muhammad (SAW), pamoja na masahaba wake wote.

 

( a ) Ipi sababu kuu ya uadui uliopo kati ya shetani na wanadamu?

 

Uadui kati ya shetani na mwanadamu ulianzia mbali mno tokea pale Allah (SWT) alipomuumba Adam (AS) na kumpulizia roho kisha akawaambia Malaika wamsujudie. Na alikua Iblisi akifanya ibada pamoja na Malaika naye akawa ni miongoni mwa walioamrishwa, lakini yeye alikataa na akafanya kiburi na wala hakusujudu.Wakati Allah (SWT) alipomwuliza sababu ya kukataa kwake kutii amri ya kumsujudia Adam (AS) alijibu kwa kusema: "Mimi ni bora kuliko yeye umeniumba kwa moto na yeye ukamuumba kwa udongo." Na hapa hasa ndio kiini cha uadui uliopo kati ya shetani na binadamu. Na picha nzuri ya historia ya uadui huo ni kama vile ilivyotolewa katika Qur-an Tukufu, Allah (SWT) anatuhadithia: "Na hakika tulikuumbeni, kisha tukakutieni sura, kisha tukawaambia Malaika msujudieni Adamu". Basi wakasujudu isipokua Ibilisi hakuwa miongoni mwa waliosujudu. Allah (SWT) akasema: "Nini kilichokuzuia kumsujudia nilipokuamrisha?" Akasema: "Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo." Akasema Allah (SWT): "Basi shuka huko, haikufai kufanya kiburi humo. Haya toka; hakika wewe ni miongoni mwa wadhalili - duni." Akasema: "Nipe muda ( nisife ) mpaka siku watakapofufuliwa viumbe." Akasema Allah (SWT): "Utakuwa miongoni mwa waliopewa muda, ( lakini si mpaka wakati huo)."Akasema: "Kwa kuwa umenihukumia upotovu basi nitawakalia waja wako katika njia yako iliyonyooka ( ili niwapoteze ), kisha nitawafikia mbele yao na nyuma yao na kulia kwao na kushoto kwao; wengi katika wao hawatakuwa ni wenye kushukuru." Akasema Allah (SWT): "Toka humo hali ya kuwa ni mwenye kudharauliwa na mwenye kufukuzwa. Atakaekufuata miongoni mwao ( nitamtia motoni ) niijaze Jahannamu kwa ninyi wote." Kisha Allah (SWT) akasema kumwambia Nabii Adam (AS): "Na wewe Adam kaa peponi pamoja na mkeo, na kuleni mnavyopenda, lakini msiukaribie mti huu msije mkawa miongoni mwa waliodhulumu nafsi zao." Basi shetani; ( naye ni yule yule Iblisi ) aliwatia wasi wasi ili kuwafichulia aibu zao walizofichiwa, na akasema: "Mola wenu hakukukatazeni mti huu ila msije kuwa Malaika au kuwa miongoni mwa wakao milele ( msife )." Naye akawaapia kwamba: "Kwa yakini mimi ni mmoja wa watoao ushauri mzuri kwenu." Basi akawateka wote wawili kwa kuwahadaa. Na walipoonja mti ule, aibu zao ziliwadhihirikia, na wakaingia kujibandika majani ya ( miti ya huko ) peponi. Na Mola wao akawaita ( akawaambia ): "Je sikukukatazeni mti huu na kukuambieni ya kwamba shetani ni adui aliye wazi?" Wakasema: "Mola wetu! Tumezidhulumu nafsi zetu, na kama hutotusamehe na kutuhurumia, bila shaka tutakua miongoni mwa wenye hasara kubwa." Allah (SWT) akasema: "Shukeni ( katika ardhi ), ninyi kwa ninyi maadui. Na makao yenu yatakuwa katika ardhi na starehe yenu pia." Al - A'raaf 11 – 23. Cha msingi tunachosoma katika aya hizi ni kwamba uadui uliopo kati ya shetani na mwanadamu hautomalizika wala kuondoka kwani yeye shetani anaona kwamba sababu ya yeye kufukuzwa kutoka kwenye neema za Allah (SWT) ni Adam. Hivyo ni lazima ampoteze yeye na kizazi chake na hii ndio sababu hasa ya Qur-an kutuhadharisha mno dhidi ya shetani huyu.

 

( b ) Ni maasi gani yanayompendeza mno Iblisi?

 

Anasema Mtume (SAW): "Hakika mamlaka ya Iblisi yapo kwenye bahari, kisha huwatuma majeshi yake, ili wawafitinishe watu. Katika fitna kubwa huja mmoja wao kumwambia, 'Nimefanya hili na lile.' Iblisi anamjibu, 'Hamna kitu.' Kisha anakuja mwingine anasema vilevile, naye humwambia pia, 'Hujafanya lolote.' Kisha anakuja mwingine anamwambia, 'Sikumuacha mtu yule mpaka nimehakiklsha ametengana na mkewe.' Hapo Iblisi humwinamia jinni huyo na kumwambia,'Wewe ndio.'" Imepokewa na Muslim.

 

WABILLAHI TAWFIQ

 

و بالله التوفيق