بسم الله الرحمن الرحيم

MAJINI

 8

Makazi ya majini, vipando vyao, elimu na maarifa waliyonayo

 

Sheikh Mustafa Mohamed Kihago

 

HOME

 

MAJINI 1 MAJINI 2 MAJINI 3 MAJINI 4 MAJINI 5 MAJINI 6 MAJINI 7 MAJINI 8 MAJINI 9

 

 Bonyeza hapa kusoma maudhui ya kila makala

 

Shukrani za dhati zimwendee Allah (SWT). Pia rehema na amani ziwe juu ya kipenzi chake Muhammad (SAW), pamoja na masahaba wake wote.

 

Ni yapi makazi ya Majini?

 

Majini wanaishi katika mgongo wa ardhi, na wanapatikana kwa wingi katika majangwa na sehemu za takataka, sehemu zenye najisi, chooni na makaburini. Na hii ndio sababu hasa ya wale waganga ambao wana uhusiano na mashetani kupenda kuwashauri wateja wao kupeleka vitu vyao na uchawi wao katika maeneo hayo.

 

Zipo hadithi za Mtume (SAW) ambazo zinakataza watu kuswali chooni, na hiyo ni kutolana na najisi iliyopo sehemu hiyo, na pia ndiyo makazi ya mashetani. Vile vile majini hupatikana kwa wingi mno katika maeneo yanayokithiri maasi kama vile masokoni. Na hiyo ndiyo sababu Mtume (SAW) akamuusia mmoja wa masahaba wake akamwambia, "Ikiwezekana usiwe ni wa mwanzo kuingia sokoni, wala wa mwisho kutoka, kwa sababu humo sokoni ndipo penye harakati za shetani, na ndipo anaposimika bendera yakc." Imetolewa na Muslim.

 

Na kama ilivyo vile vile mashetani hukaa katika majumba ya binadamu, na Bismillahi tu ndiyo inayowakimbiza. Amepokea Muslim na Abu Dawood kutoka kwa Jabir kwamba Mtume (SAW) amesema: "Yeyote atakayeingia nyumbani kwake akataja jina la Allah (SWT) wakati anaingia na wakati anapokula shetani husema: ‘Leo hapana malazi hapa wala chakula’, na atakapomtaja Allah (SWT) wakati anapoingia nyumbani, na asitaje wakati wa kula, shetani husema, 'Mmewahi chakula lakini hakuna kulala', na mtu asipotaja jina la Allah (SWT) anapoingia nyumbani kwake shetani husema kuwaambia wenzake, ‘mmewahi chakula na malazi’."

 

Na mahali pengine ambapo shetani hupenda kukaa `ni kati ya jua na kivuli', na hiyo ndio sababu ya Mtume (SAW) kutukataza kukaa katika sehemu hizo, kama ilivyopokewa katika hadithi.

 

 

Vipando vya majini?

 

Mtume (SAW) ameelezea kwamba majini nao wana vipando, na hiyo ni katika hadithi sahihi iliyotolewa na Muslim kutokana na Ibn Mas'ud (RA) kwamba Majini walimwomba Mtume (SAW) awaombee chakula, ndipo Mtume (SAW) akasema: "Mtakula kila mfupa uliotajwa jina la Allah (SWT) ambao utakua ni bora kuliko nyama, na kila samadi itakua ni chakula cha vipando vyenu." Katika hadithi hii kuna dalili ya wazi ya kuonyesha kwamba Majini nao wana vipando.

 

Elimu na maarifa waliyonayo Majini

 

Kuna baadhi ya watu ambao wanadai kutibu wagonjwa na kwamba wao wamejifunza tiba hiyo kupitia kwa majini. Na kweli tokea zamani tunasikia kwamba kuna watu wa namna hii wanye uwezo wa kutibu baadhi ya maradhi sugu kama yanavyofahamika. Na miongoni mwa visa vinavyofahamika ni kile kilichosimuliwa na An-nadr bin Amril-Harithiy, aliposema: "Katika zama za ujahiliyah tulikua siku moja karibu na kisima, nikamtuma binti yangu na chombo ili anitekee maji, akakawia, tukamtafuta lakini hatukumwona mpaka tukakata tamaa. Akasema: 'Naapa kwa Allah (SWT) kwamba siku moja nilikua nimekaa mbele ya baraza yangu, akanitokezea Sheikh mmoja, alipoinama kuniangalia mara akawa ni binti yangu. Nikasema: 'Binti yangu.' Akasema: 'Binti yako ndiyo!' Nikasema: 'Ulikua wapi binti yangu?' Yule binti akasema, 'ile siku uliponituma kisimani, alinichukua jinni akawa ananizungusha huku na kule, nikawa nipo kwao mpaka ilipotokea vita kati ya makundi mawili ya majini. Akaahidi kwamba wakishinda vita atanirudisha. Wakashinda ndipo aliponirudisha.' Lakini akawa binti huyo amebadilika rangi yake ya mwili na akawa amekonda sana. Akakaa kwa muda akaanza kubadilika kuwa katika hali ya kawaida, akachumbiwa na mabinamu zake tukamwozesha. Lakini lile jinni likawa limempa ishara ya kumwita kwa moshi pindi panapotokea matatizo yeyote. Basi yule mume wake akawa anamkera na kumwambia wewe ni jini, shetani wala si mtu. Basi yule binti akawasha moshi, yule mume akasikia sauti inamwambia, 'Una nini na huyu ukimsogelea atakutoboa jicho. Nimemchunga tokea wakati wa ujahiliyah kwa maarifa yangu, na katika uislam kwa dini yangu.' Yule mume akamwambia, 'Huwezi ukajitokeza tukakuona?' Yule jinni akajibu, 'Haturuhusiwi. Hakika baba yetu aliomba mambo matatu. Tuone lakini tusionekane, tukae katika tabaka za ardhi, na aishi mmoja wetu mpaka atakapofikia kuwa mtu mzima, kisha atarudi tena kuwa kijana mdogo.' Yule bwana akamwuliza: 'Je unaweza kunipa dawa ya homa?' Lile jinni likajibu: 'Ndio. Unamjua yule mdudu mdogo katika maji, ambaye anafanana na buibui?' Yule bwana akasema, 'Namfahamu.' Basi yule jinni akamwambia, 'Mchukue halafu tengeneza nyuzi kutokana na miguu yake kisha ufunge katika mkono wako wa kushoto.' Yule bwana akafanya hivyo. Akawa kama aliyefunguliwa kamba ya shingo."

 

Pia Zayd bin Wahab alisema, "Tulipigana vita tukashuka katika kisiwa kimoja, wakawasha moto, pakawa pana chumba kikubwa, akasema mmoja wao, 'mimi naona kuna chumba kikubwa, pengine mnawaudhi waliomo ndani ya chumba hiki.' Wakazima moto wao. Akatokezewa usiku akaambiwa, 'Hakika wewe umeihami nyumba yetu tutakufundisha tiba ambayo itakusaidia, atakapokujia mgonjwa basi chochote utakachomwambia kuwa ni dawa basi atapona.' Ikawa siku moja akajiwa na mtu mwenye tumbo kubwa, alipokua amekaa katika msikiti wa Kufah. Yule mtu akamwomba ampatie dawa ya tumbo lake. Akamwambia, 'Hivi jamani hamshangai kumwona mtu ananiuliza kuhusu dawa naye atakufa leo kwa kula matunda?' Basi siku ile ilipopita watu wakamfuata kumwambia, 'Wewe ni mwongo mbona yule bwana hajafa?' Akawaambia, 'Muulizeni hali ya ugonjwa wake.' Wakasema amekwisha pona.' Akawaambia, 'Mimi nilimtisha asile sana!' Kimetolewa na Abadalla bin Muhammad A-Qurashiy.

 

WABILLAHI TAWFIQ

 

و بالله التوفيق