بسم الله الرحمن الرحيم

MAJINI

HABARI ZA MAJINI KUTOKANA NA QUR-AN NA SUNNAH

HOME

MAJINI 1 MAJINI 2 MAJINI 3 MAJINI 4 MAJINI 5 MAJINI 6 MAJINI 7 MAJINI 8 MAJINI 9

Bonyeza hapa kusoma maudhui ya kila makala

UTANGULIZI

Bila shaka shukrani zote zimwendee yule aliyemwumba mwanadamu kwa udongo kama mfinyanzi, na kisha kaumba majini kutokana na ncha ya moto, na kuwafanya majini hao ni kificho, wasiweze kuonekana kwa macho, akaweka ya kwamba wapo wema miongoni mwao na wapo waovu, na hakuweka utawala wa majini uwe juu ya binadamu, isipokuwa tu ile hali ya wasiwasi inayosababishwa na Shetani.

Pia rehema na amani ziwendee Mtume wetu Muhammad (SAW) aliyepelekwa na Allah (SWT) kwa watu wote na viumbe vyote. Akapelekewa (SAW) kundi la majini kwa ajili ya kusikiliza Qur-an, na pindi walipohudhuria ( hiyo Qur-an ) majini hayo yalisema kuambiana : Nyamazeni! Na pindi ilipokwishasomwa majini hao walienda kwa wenzao wakawaonya na kuwahadharisha. Vile vile Allah (SWT) akamfunulia Mtume wetu Muhammad (SAW) kwamba kuna kundi la majini lilisikiliza Qur-an likasema : Hakika sisi tulisikia Qur-an ya ajabu, yenye kuelekeza katika uongofu, nasi tukaiamini, na hatutomshirikisha Allah (SWT) na yeyote yule.

Ama baada ya yaliyotangulia; Ulimwengu wa majini umejaa maajabu na siri nyingi, kwa hivyo basi, watu wengi wana shauku ya kuujua ulimwengu huu na siri zake. Kuna maswali mengi yanayoulizwa kuhusiana na ulimwengu huu wa majini, kwani watu wengi wanazozana tokea zamani hadi leo hii kuhusu kuwepo kwa majini au kutokuwepo. Jambo hili limezungumzwa vizuri mno katika dini yetu ya Kiislam kwani Qur-an Tukufu imeeleza kwa kina kuhusu kuwepo viumbe wanaofahamika kama Majini ambapo wapo majini wema ( wacha Mungu ) na wabaya ambao ndio mashetani. Hivyo basi tumeamua kuandaa WEBSITE hii ambayo inakusanya makala tulizokuwa tukizitoa katika Masjid Quba, Arusha, kuanzia Desemba mwaka jana ( 2002 ) ili kujibu maswali mengi ambayo yanayoulizwa na watu wengi. Ni nia yetu Inshaallah kuzikusanya hizi makala katika kitabu huko mbeleni na pia tutaweka hicho kitabu katika WEBSITE hii.

Elimu hii ya majini imekusudiwa hasa kutoa ulinganio wa Tawheed, ibada ya kumpwekesha Allah (SWT), pia kukataza mambo ya bid’aa na ushirikiano ambao yameenea mno ulimwengu mzima. Vile vile siri ya ulimwengu huu wa majini hauwezi kujulikana isipokuwa tu kwa kuzama zaidi katika jambo hili kwa undani zaidi.

Maudhui ambazo tutazizungumzia ni kama zifuatazo :

1. Uhakika wa kama kweli upo Ulimwengu wa majini
2. Majukumu waliopewa majini na Allah (SWT)
3. Majini katika maisha yao ya kibinafsi
4. Majini na elimu
5. Majini na Mitume
6. Mambo ya majini huku na kule
7. Ugomvi uliyopo kati ya Shetani na mwanadamu
8. Silaha ya kupambana na Shetani

Hivyo msomaji atapata ukweli kuhusiana na maisha ya majini, ambapo yote tutakayoyaeleza yatatokana na kitabu cha Allah (SWT) Qur-an, pamoja na Sunna za Mtume Muhammad (SAW), vile vile kauli mbali mbali za wanazuoni ili kutufichulia siri ya ulimwengu huo.

Tumejitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kuelezea kila kitu bayana, wepesi na kwa ukweli…….. na Allah (SWT) ndiye mkusudiwa……naye ndiye tegemezi langu.

Al – Ustadh Sheikh Mustafa Mohamed Kihago
Arusha, Tanzania

Muharram, 8, 1424, March, 11, 2003